Semi ni nini?
- Tungo fupi zinazowasilisha ujumbe kwa kufumba au kuchora picha.
Sifa
- Huwa fupi kwa kuwasilisha ujumbe mrefu kwa maneno machache
- Ni tanzu tegemezi kwa hutegemea tanzu nyingine kama vile hadithi, mazungumzo, n.k.
- Hazibadiliki vivi hivi
- Baadhi ni kielelezo cha maadili k.v. methali
- Hutumia lugha ya kimafumbo
- Huibua taswira
- Huwa na mchezo wa maneno
- Baadhi huwa na muundo maalum k.v. methali na vitendawili
- Nyingine ikikosa kutumika hutoweka k.v. misimu
Umuhimu
- Kuonya k.m methali, ‘Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.’
- Kukuza uwezo wa kufikiri k.m. vitendawili na chemsha bongo
- Kutafsidi lugha au kupunguza ukali wa maneno k.m. nahau ‘jifungua’ badala ya ‘zaa’
- Kuburudisha k.m. vitendawili, chemsha bongo na vitanza ndimi
- Kuhifadhi siri k.m. nahau, misemo, misimu
- Kuelimisha k.m. kutofanya mambo kwa pupa-mla kwa pupa hadiriki kula tamu
- Kuongeza utamu katika lugha
- Kuboresha matamshi k.m. vitanza ndimi
- Kukuza lugha k.m misimu
- Kukuza utangamano katika jamii kwa kuleta watu pamoja wakati zinawasilishwa
Vipera vya Semi
a) Methali
- Semi fupi ambazo hueleza kwa muhtasari au mafumbo ukweli fulani wa kimaisha.
Sifa
- Huwa fupi k.m. ‘Msafiri kafiri.’
- Hutumia tamathali za usemi.
- Hutumkia lugha ya kimafumbo.
- Huwa na maana ya ndani na nje.
- Kunazo hufanana kimaana k.m. ‘Haraka haraka haina baraka’ na ‘Polepole ndio mwendo.’
- Hupingana zenyewe k.m ‘Polepole ndio mwendo’ na ‘Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako.’
- Huwa na sifa za kishairi k.v. ukwapi, utao na vina -Haba na haba, hujaza kibaba.
- Sifa za utegemezi kwa kuingiliana na tanzu nyingine za fasihi
- Huwa na muundo maalum wa sehemu mbili:
i) Wazo k.m ‘Haba na haba…’
ii) Kukamilisha wazo ‘…hujaza kibaba.’
Umuhimu
- Kukuza uwezo wa kufikiri kwani mpokezi hufikiri ili kupata maana ya ndani
- Kuonya dhidi ya matendo yasiyofaa k.m. Mchimba kisima huingia mwenyewe na Ukiambiwa jiambie usijeishia kumbe.
- Kufariji walio katika hali ngumu, k.m Baada ya dhiki faraja, Hakuna marefu yasiyo na ncha, Liandikwalo ndilo liwalo, Ajaliwalo ndilo apatalo
- Kuhimiza watu kujitahidi maishani/kuonyesha jambo jema huja kwa kufanyiwa kazi k.m. Mtaka cha mvunguni sharti ainame, Chumia juani ulie kivulini
- Kupamba lugha iwe na mvuto kwani huwa na usanii mkubwa
- Kuhimiza ushirikiano k.m. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, Jifya moja haliijiki chungu
- Kuelimisha mtu ajue jambo muhimu k.m. Usione kwenda mbele kurudi nyuma si kazi, Pema usijapo pema ukipema si pema tena
- Kushauri k.m. Enga kabla ya kujenga na Mchama ago hanyeli
- Kufupisha maadili katika ngano
- Kubuni lakabu k.m. kikulacho
- Kufunza maadili k.m. kuwa na subira - Subira huvuta heri.
- Kuhimiza kutokata tama k.m. Bandu bandu huisha gogo, Papo kwa papo kamba hukata njiwe
- Kuonyesha umuhimu wa kuthamini jamaa zako kuliko marafiki k.m. Damu ni nzito kuliko maji, Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe
- Kuonyesha umuhimu wa kuthamini vitu vyako - Usiache mbachao kwa msala upitao na Afadhali dooteni kama ambari kutanda
- Kukashifu ubinafsi k.m. Mwamba ngoma huvutia kwake, Kila mchukuzi husifu mzigo wake
- Kukashifu kiburi k.m. Maskini akipata matako hulia mbwata, Zingwi zingwi lipe nguo utaona mashauo
Mbinu za Lugha/Fani /Tamathali za Usemi katika Fasihi
- Maneno au vifungu vya maneno vinavyotumiwa kutia fasihi urembo ili kufanya ujumbe ueleweke vyema zaidi.
- Tashbihi - Ulinganishi kwa kutumia viunganishi kama, mithili, mfano na sawa k.m Kawaida ni kama sheria
- Sitiari/ Istiara - Ulinganishi usio wa moja kwa moja k.m Mgeni ni kuku mweupe
- Tashhisi/Uhaishaji - Kukipa kitu sifa ya uhai k.m Siri ya mtungi muulize kata
- Taashira/ Ishara - Kitu kuwakilisha kingine k.m Kimya kingi kina mshindo mkubwa
- Chuku/udamisi - Kutia chumvi au kufanya kitu kionekane kikubwa sana au kidogo sana k.m Usipoziba ufa utajenga ukuta
- Takriri - Urudiaji wa neno au mafungu ya maneno k.m Haba na haba hujaza kibaba
- Tanakuzi - Maneno yaliyo kinyume k.m Mpanda ngazi hushuka
- Tabaini - Msisitizo kwa njia ya kinyume kwa kutumia kikanushio 'si'
- Ritifaa - Kusemesha asiyekuwapo kama yupo
- Taharuki - Kuacha msomaji akiwa na hamu ya kutaka kujua kipi kitakachojiri halafu
- Mbinu rejeshi - Kukumbusha mambo yaliyopita k.m
- Balagha - Maswali yasiyohitaji majibu k.m Pilipili usiyoila yakuwashiani?
- Taswira - Ujenzi wa picha akilini k.m Mpanda farasi wawili hupasuka msamba
- Kinaya - Mhusika kutumia maneno au matendo yaliyo kinyume cha inavyotarajiwa k.m Asante ya punda ni mateke
- Kejeli - Kudharau au kubeza k.m Ucha Mungu si kilemba cheupe
- Jazanda - Kufananisha vitu kwa mafumbo k.m. katika biblia k.m Kupanda mchongoma kushuka ndio ngoma
- Kweli kinzani - Hoja mbili zinazopingana/kutowezekana k.m Wagombanao ndio wapatanao
Vigezo vya Kuainishia Methali / Kuziweka Pamoja na kuzichambua
- Mandhari/mazingira k.m. kilimo. k.m Ukipanda pantosha utavuna pankwisha
- Maudhui k.m. ulezi k.m Samaki mkunje angali mbichi
- Fani/tamathali k.m Haba na haba hujaza kibaba
- Jukumu k.m. kuonye k.m Asiyesikia la mkuu huvunjika guu
- Maana k.m. sawa k.m Haraka haraka haina baraka
ii) Vitendawili
- Semi ambazo hutolewa kwa mtu kwa mfano wa swali ili azifumbue.
Sifa
- Huwa vifupi kimaelezo.
- Hutumia lugha ya kimafumbo.
- Hutolewa mbele ya hadhira.
- Hutumia ufananisho wa kijazanda.
- Kunazo huhusiana na methali k.m. mzee amekufa vyombo vimevunjikavunjika.
- Huwa na wakati maalum wa kutolewa yaani jioni.
- Huwa na mchezo wa maneno k.m. Ukiona njigi utadhani njege
- Hujisimamia vyenyewe
- Kunavyo huwa na jibu zaidi ya moja
- Hutumia tamathali za lugha kwa ufanifu mkubwa
- Huweza kuwa na fomyula/muundo maalum
-
k.m. Mteguaji: Kitendawili
Mteguaji: Tega
Umuhimu
- Kuburudisha jioni baada ya kazi
- Kukuza ubunifu wa kuvitunga kwa kulinganisha vitu katika mazingira ili kuviunda
- Kuimarisha uwezo wa kukumbuka
- Kukuza uwezo wa kufikiri kwani mfumbiwa huhitaji kufikiri sana ili kupata jibu
- Kuleta umoja na ushirikiano katika jamii kwa kuleta watu pamoja wakati vinategwa
- Kuimarisha ujuzi wa kujieleza kwa lugha
- Kupanua ujuzi wa mazingira wa mtoto
- Kuendeleza utamaduni wa jamii k.m. Nyumbani mwetu mna papai lililoiva lakini. siwezi kulichuma
- Kukejeli au kudharau tabia mbaya k.m. Wazungu wawili wanachungulia dirishani