- Hadithi ni masimulizi yanayotumia lugha ya mtiririko au nathari
Sifa
- Hutumia ya lugha ya mtiririko au nathari- kueleza matukio moja kwa moja
- Hurithishwa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine
- Huwasilishwa mbele ya hadhira
- Hutambwa mahali maalum k.v. ndani ya nyumba, chini ya mti, uwanjani, n.k.
- Huweza kutokana na matukio halisi (kihistoria) au ya kubuni
- Huwa na mafunzo fulani kwa jamii/hadhira
- Hutumia wahusika wa aina tofauti k.v. nyumbani, wanyama, ndege, mazimwi, n.k.
- Hutumia aina nyingine za sanaa k.v nyimbo, methali, ushairi, n.k.
- Huwa na utendaji k.v. mtambaji kuiga fisi anavyokula
- Aghalabu hutambwa jioni
Majukumu ya Hadithi
- Kufunza maadili yaliyo nguzo kuu kwa wanajamii
- Kukuza ujasiri wa kuzungumza hadharani
- Kuburudisha baada ya kazi ya kutwa
- Kukuza uwezo wa watoto wa kukumbuka ili kutamba baadaye
- Kueleza asili ya mambo k.m visaviini, visasili na ngano za usuli
- Kutahadharisha wanajamii dhidi ya kufanya mambo yasitofaa
- Kuunganisha watu katika jamii wanapojumuika pamoja kusikiliza utambaji
- Ngano za mtanziko hukuza uwezo wa kutathmini na kutoa uamuzi ufaao
- Kukuza lugha hasa kwa hadhira ya watoto
- Kuhifadhi na kuendeleza historia ya jamii k.v. mighani, tarihi, n.k.
- Kuelimisha hadhira kuhusu utamaduni wao
- Njia ya kupokeza kizazi historia na utamaduni wa jamii
Sifa za Mtambaji / Mganaji Bora
- Asiwe mwoga ili kuweza kuzungumza hadharani.
- Asiwe na haya ili kuweza kuzungumzia mambo ya aibu inapobidi
- Awe na uelewa wa mazingira na masuala ibuka katika jamii ili kuweza kuwasilisha dhana zisizopatikana katika mazingira yake k.m. kutumia rais kuelezea dhana ya mfalme
- Awe na ufahamu mpana wa lugha ili aweze kuitumia kwa uhodari na kuwasilisha kwa wepesi
- Awe mchanganfu na mcheshi ili kunasa makini ya hadhira na kuzuia isikinai
- Awe na ufahamu mpana wa utamaduni husika ili kuzuia kutumia maneno na ishara zinazoweza kuwaudhi au kupingana na imani za hadhira
- Awe na uwezo wa kushirikisha hadhira k.v. kuimba, maswali ya balagha ili isikinai, n.k.
- Aweze kujua, matarajio, kiwango cha elimu na tajriba ya hadhira ili kuweza kubadilisha kwa kiwango kinachofaa
- Awe na uwezo wa kuingiliana vizuri na hadhira ili aivutie
- Awe na kumbukumbu nzuri ili usimulizi wake utiririke vizuri
- Awe na uwezo wa kudramatisha ili kuonyesha picha fulani k.v. kuiga toni, sauti, na kiimbo kulingana na swala analowasilisha
- Kubadilisha toni au kiimbo ili hadhira isikinai
- Awe na ujuzi wa kutumia ishara za uso, mwili na miondoko kulingana na hali anayoigiza
- Awe na ujuzi na ufasaha wa lugha ili kuwasilisha mawazo kwa njia mwafaka na inayovutia
- Aweze kubadilisha toni na kiimbo kulingana na hali tofauti anazoigiza k.v. huzuni
- Awe na uwezo wa kushirikisha hadhira kwa nyimbo na maswali ya balagha ili kuondoa uchovu wa kutazama na kusikiliza
- Awe na uwezo wa ufaraguzi/ kubadilisha utambaji wake papo hapo kutegemea hadhira yake na kutoa mifano inayofahamika kutoka katika mazingira ya hadhira
- Awe na uwezo wa kutumia mtuo wa kidrama ili kuongeza taharuki, kusisitiza ujumbe na kuteka makini ya hadhira
Aina za Hadithi
- Kuna aina mbili za hadithi
- Hadithi za Kubuni / Ngano - Hazisimulii matukio ya kweli bali ya kutungwa
- Hadithi za Kisalua/Kihistoria - Zinazosimulia matukio yaliyowahi kutendwa na wahusika waliowahi kuishi. Huongezewa ubunifu ili kuvutia zaidi.
Hadithi za Kubuni / Ngano
- Hadithi zinazosimulia kisa chenye funzo na zenye wahusika aina ya binadamu, viumbe na vitu visivyo na uhai.
Sifa za Ngano
- Zina fomyula ya kuanzia/mwanzo maalum
- Zina fomyula ya kumalizia/mwisho maalum
- Zina wahusika aina mbalimbali
- Zina matumizi ya nyimbo
- Hutumia takriri (usambamba) ili kusisitiza k.m. zimwi likakimbia, likakimbia
- Huwa na na maadili/mafunzo
- Hutumia maswali ya balagha kuongeza taharuki
- Hutumia tanakali za sauti
- Zina matumizi ya fantasia au matukio yanayokiuka uhalisi/mambo ya ajabu k.v. binadamu
Aina za Fomyula za Kuanzia/Mianzo Maalum
- Paukwa, Pakawa. Sahani. Ya mchele. Giza. La mwizi. Na kiboko je? Cha mtoto mkorofi...
- Hapo zamani za kale/za kongamawe...
- Ilitokea...
- Hadithi! Hadithi! Hadithi njoo...
- Kaondokea chenjangaa, kajenga nyumba kakaa, mwanangu mwanasiti, kijino kama chikichi, cha kujengea kikuta, na vilango vya kupita...
- Hapo jadi na jadudi...
Umuhimu wa Fomyula ya Kuanzia/Mwanzo maalum
i) Kuvuta makini ya hadhira
ii) Kumtambulisha mtambaji kwa hadhira
iii) Kuashiria mwanzo wa hadithi
iv) Kutoa hadhira kutoka ulimwengu halisi hadi ule wa hadithi
Aina za Fomyula za Kumalizia/Miishio Maalum
- Hadithi inaishia hapo.
- Tangu siku hiyo...
- Wakaishi raha mustarehe.
- Maadili
Umuhimu wa Fomyula ya Kumalizia/Mwisho Maalum
i) Kuashiria mwisho wa hadithi.
ii) Kutoa hadhira katika ulimwengu wa hadithi hadi ule halisi.
iii) Kumpisha/kumpa fursa mtambaji anayefuata.
iv) Kupisha shughuli inayofuata.
v) Kutoa funzo la hadithi kwa muhtasari.
vi) Kupa hadhira nafasi ya kupumzika baada ya kuwa makini kwa muda
Umuhimu wa Nyimbo katika Ngano
i) Kushirikisha hadhira.
ii) Kusisimua hadhira na kuondoa ukinaifu
iii) Kuteka makini yao.
iv) Kuwasilisha mafunzo/maadili.
v) Kutenganisha matukio katika hadithi.
vi) Kuburudisha hadhira.
vii) Kupunguzia hadhira mwemeo.
Umuhimu wa Tanakali za Sauti/Onomatopeya katika Ngano
i) Kuongeza utamu.
ii) Kusaidia msomaji kupata picha kamili.
iii) Kusaidia kupata hisia halisi
Aina za Ngano (Hadithi za Kubuni)
i) Hurafa
- Hadithi zenye wahusika wanyama na ndege.
- Hurafa za kijanja ni hadithi ambapo wanyama wadogo hutumia ujanja wa hali ya juu ili kujinasua na hali ngumu au mitego wanayotegewa
Sifa
- Wahusika ni wanyama au na au ndege
- Wanyama na ndege hupewa sifa za binadamu
- Ni kazi ya ubunifu
- Hutoa mafunzo kwa njia ya kuchekesha na isiyoumiza
- Huwa na ucheshi mwingi
- Hutumia mbinu ya uhuishi
- Huwa na sifa zinazohimizwa na zinazoshutumiwa
- Ujanja au uongo hujitokeza katika hurafa za kijanja
- Ushindi hujitokeza katika hurafa za kijanja
Umuhimu
- Kutahadharisha watu dhidi ya kuwa wa danganyifu/kudanganyika kwa urahisi
- Kuonyesha jinsi tabia ya udanganyifu inavyoweza kujitokeza na kuathiri watu
- Hurafa za kijanja hufunza jinsi ya kupampana na hali ngumu
ii) Hekaya/Ngano za Kiayari
- Hadithi zinazomsawiri mhusika anayetumia ulaghai kupata matilaba yake kutoka kwa wengine (kwa mfano: Abunuwasi).
Sifa
- Wahusika wakuu ni binadamu
- Huwa na ubunifu mkubwa
- Hustaajabisha na kuchekesha
- Ujanja na uongo hujitokeza
- Ushindi hujitokeza
- Ni za kubuni
Umuhimu
- Hutahadharisha watu dhidi ya kuhadaika kwa wepesi
- Huonya dhidi ya matokeo yanayoweza kuwapata wanaojinyakulia mali kwa udanganyifu
- Kuonya dhidi ya usaliti
- Kukashifu viongozi dhalimu na matendo maovu
- Kukejeli wanaotumia nguvu badala ya akili/hekima
iii) Visasili
- Hadithi zinazoeleza asili ya matukio fulani katika jamii k.m. kifo, jua, lugha, zilizala n.k.
Sifa
- Husimulia mambo ya kiimani na kidini
- Huwa na misingi ya kihistoria
- Hueleza asili ya matukio katika jamii
- Wahusika ni wanyama na binadamu
- Huwa na maadili
- Hurithishwa kizazi hadi kingine
Umuhimu
- Kueleza asili ya mambo kama vile kifo, utamaduni n.k.
- Kueleza utaratibu wa kutekeleza desturi k.v. mahari
- Kuhalalisha baadhi ya mila na desturi za jamii k.v. ulipaji mahari, uabudu miti, n.k.
- Kukitisha mizizi imani fulani ya watu
- Kupunguza athari za majanga kama vile kuhalalisha kifo
- Kutambulisha jamii kwani kila jamii ina aina yake ya visasili
- Kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii
iv) Ngano za usuli
- Hadithi zinazoeleza asili ya hali, tabia, mahusiano au wasifu. k.v. asili ya kuku kuchakura, asili ya kinyonga kwenda kwa tahadhari, n.k.
Sifa
- Wahusika ni wanyama na binadamu
- Ni kazi ya kubuni
- Hueleza kuhusu asili ya sifa, tabia au hali.
- Hutumia mbinu ya uhuishi
- Huwa na maadili
Umuhimu
- Kueleza sababu ya tabia, hali au sifa Fulani
- Kuonya dhidi ya tabia hasi kama vile ulafi
v) Ngano za mazimwi
- Hadithi ambazo wahusika ni mazimwi.
Sifa
- Wahusika ni mazimwi
- Mazimwi huwakilisha sifa hasi za binadamu k.m ulafi, ukatili, uovu n.k.
- Hujaa uharibifu
- Huwa na matumizi mengi ya fantasia
- Kipengele cha safari hujitokeza k.v. kwenda nchi za mbali kutafuta suluhisho.
- Ushindi hujitokeza (mazimwi hushindwa)
- Ni kazi ya kubuni
- Huwa na maadili
- Mazimwi huwa na sifa zinazokiuka mipaka ya binadamu k.m. kinywa kisogoni, jicho moja kubwa, n.k.
Umuhimu
- Kukashifu tabia ya uovu, ulafi, na ukatili
- Kutahadharisha dhidi ya kuwa na ulafi, ukatili n.k.
- Kutia moyo waliodhulumiwa kuwa waliowanyanyasa wataadhibiwa siku moja
vi) Ngano za Mashujaa
- Ambazo zinazohusu watu waliotenda matendo ya kishujaa katika jamii zao kama vile kuokoa jamii.
- Ngano za mashujaa ni za kubuni ilhali katika mighani, mashujaa wanaaminiwa waliishi.
Sifa
- Kipengele cha motifu au kusafiri nchi za mbali, kupigana na mazimwi kuokoa jamii
- Husawiri mapigano kati ya wema (lila) na ubaya (fira)
- Uovu huwakilishwa na mazimwi au viongozi dhalimu
- Hatimaye wema hushinda uovu kwa juhudi za mashujaa
Umuhimu
- Kuhimiza uzalendo na ujasiri miongoni mwa vijana
- Kuhimiza ujasiri miongoni mwa vijana
- Kusifu mashujaa katika jamii
- Kuelimisha jamii kwa kuwapa maarifa ya kukabiliana na changamoto, inda na ila
- Kuhimiza uzalendo kwa kuhimiza watu kuiga mashujaa na kupigania jamii
- Kuonya dhidi ya matendo hasi k.v. ukatili
- Kuhimiza watu kutokata tamaa
vii) Ngano za mtanziko
- Hadithi ambapo mhusika hukabiliwa hali ngumu ya kuamua baina ya mambo wawili au zaidi yanayomkabili.
Sifa
- Wahusika ni wanyama au binadamu
- Ni kazi ya kubuni
- Mhusika hulazimika kufanya uteuzi mgumu
- Hali mbili au zaidi zinazotatanisha huwepo
Umuhimu
- Hutuerevusha jinsi ya kupambana na hali ngumu
- Kuonya/kutahadharisha dhidi ya kujiponza
- Kukuza uwezo wa kupima mambo na kuteua lililo muhimu
- Kuonya dhidi ya kutenda bila kuwaza kwa kina
viii) Ngano za Kimafumbo
- Ambazo huwa na maana ya ndani/iliyofichika.
- Istiara - Hadithi ambayo maana yake huwakilisha maana nyingine iliyofichika k.v. hurafa ambapo wanyama huwakilisha binadamu
- Mbazi - Hadithi fupi inayotolewa inayotolewa kama mfano kumkanya au kumwelekeza mtu k.v. katika biblia
Hadithi za Kisalua/Kihistoria
i) Mighani
- Hadithi za mashujaa/majagina wa jamii fulani k.m. Rwanda Magere wa Waluo, Fumo Liyongo wa Wapate, Koome Njue wa Wameru, Wangu wa Makeri wa Wakikuyu na Syokimau wa Wakamba.
Sifa
- Huhusu mashujaa wa jamii fulani
- Wahusika hupambana na hali ngumu inayosababishwa na maadui
- Wahusika hupewa sifa na uwezo usiokuwa wa kawaida k.v. ukubwa wa ajabu, nguvu katika kivuli, nguvu katika nywele, kutoulika n.k.
- Wahusika hupigania haki za wanyonge
- Mhusika hukomboa jamii yake dhidi ya maadui
- Mhusika hufa kifo cha huzuni (tanzia) kwa kusalitiwa na mtu wa karibu k.v. mwanamke au jamaa zao
- Mashujaa huuliwa kwa njia ya ajabu kama vile kunyolewa nywele, kivuli kuchomwa mkuki, kuchomwa shindano ya shaba kitovuni
- Mighani huzungumzia matukio ya kihistoria
- Kuna tabia ya kupiga chuku matukio yaliyo hadithini
- Mighani hurithishwa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine
- Huchukuliwa na jamii kama hadithi zenye ukweli na jamii hujinasibisha na mighani hiyo
- Husimulia mambo ya kiimani na kidini
Umuhimu
- Kutambulisha jamii kwani kila jamii ina aina yake ya mighani
- Kuhifadhi na kumbusha historia yajamii
- Kusifu mashujaa katika jamii
- Kuhimiza ujasiri miongoni mwa vijana
- Kuelimisha jamii kwa kuwapa maarifa ya kukabiliana na adui au changamoto
- Kukuza uzalendo kwa kuhimiza watu kuiga mashujaa na kupigania jamii
- Kuonya dhidi ya matendo hasi kama vile usaliti
- Kuhimiza watu kutokata tama
ii) Visakale
- Masimulizi ya matukio yaliyotendeka zamani k.v. vita, majanga kama njaa na magonjwa na hamahama za jamii k.v. waisraeli kutoka misri
iii) Visaviini
- Hadithi zinazoeleza chimbuko la jamii Fulani
iv) Mapisi
- Maelezo ya kihistoria yasiyo na ubunifu wowote k.v. chimbuko la kundi la wabantu kutoka Afrika ya Kati na kuenea sehemu mbalimbali za Afrika
v) Tarihi
- Maelezo kuhusu matukio ya kihistoria kulingana na yalivyofuatana ki wakati
vi) Kumbukumbu
- Maelezo ya kitawasifu kuhusu mtu au jamii inayotambulika kwa kutoa mchango fulani mkubwa
Vipera Vingine vya Hadithi
i) Soga
- Hadithi fupi za kuchekesha zinazolenga kutania au kudhihaki
Sifa
- Wahusika ni wa kubuni
- Hutaja ukweli unaoumiza
- Hutumia vichekesho kupunguza ukali wa dhihaka
- Hutumia chuku kupita kiasi
- Huhusu tukio moja
- Ni fupi
Umuhimu
- Kukashifu matendo hasi kwa njia ya ucheshi
- Kuonya na kutahadharisha dhidi ya matendo hasi k.v. ulaghai
- Kufunza maadili
- Kuburudisha kwa kuchekesha
ii) Vigano
- Hadithi fupi zinazosimulia kuhusu matendo mabaya katika jamii na wakati uo huo kuonya na kuelekeza dhidi yayo.
- Aghalabu huandamana na methali kwa lengo la kufafanua linalokusudiwa au kudhibitisha funzo la methali fulani.
Sifa
- Huwa vifupi
- Husimulia kisa kimoja tu
- Wahusika ni binadamu na wanyama
- Hufunza maadili kutokana na methali
iii) Kisa
- Masimulizi mafupi yenye tukio moja lenye funzo kwa njia ya kufurahisha
Mambo ya Kuzingatia katika Uchambuzi wa Hadithi/Ngano
- Tanzu ni aina za tungo zenye muundo uliokaribia kufanana.
- Kueleza aina ya ngano kwa kuzingatia wahusika na maudhui
a) Ngano yaweza kuwa ya mazimwi na ya mashujaa kwa wakati mmoja
b) Ngano yaweza kuwa hurafa, ya usuli na ya kiayari
- Kutaja wahusika
- Kufafanua sifa za wahusika wakuu
- Maadili/mafunzo yanayojitokeza katika hadithi
- Kubainisha sifa za ngano/hurafa/hekaya, n.k. zinazojitokeza katika hadithi
- Kueleza umuhimu wa fomyula ya kuanzia/wimbo uliotumiwa katika hadithi
- Kubainisha tamathali za usemi zilizotumiwa katika hadithi fulani
- Kuonyesha jinsi ngano inavyoshughulikia maudhui fulani
- Kufafanua ufaafu wa methali fulani zilizotumiwa katika hadithi
- Katika ngano ya mtanziko, ungekuwa mhusika mkuu ungefanya nini?
- Kubainisha matumizi ya mbinu ya fantasia
- Kufafanua maswala ibuka/maudhui yaliyoshughulikiwa k.m. usaliti, ujinga, ulaghai, n.k.
- Kuchanganua utungo kifani-ploti, wahusika, mbinu za lugha, fantasia, nyimbo, n.k.
- Kueleza majukumu ya hadithi